Friday , 8th Jun , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kali wananchi wote wanaotumia vibaya namba za mawasiliano za jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu matukio ya majanga ya moto.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo wakati alipofanya ziara katika Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura ya Maafa pamoja na Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha mkoa wa Ilala.

"Ili kudhibiti wananchi wanaopiga simu za kuomba msaada wa kutaka kuokolewa, huku kukiwa hakuna tukio lolote la janga la moto lililotokea kwenye maeneo yao, ni vema watu hao wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo", amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo baada ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,  Thobias Andengenye kumweleza baadhi ya changamoto zinazolikabili jeshi hilo kuwa ni pamoja na wananchi kupiga simu wakidai kuna ajali ya moto imetokea katika maeneo yao na baada watu wa uokoaji kufika wanabaini ni uongo.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini kuendelea kutoa mafunzo kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na kupambana na majanga ya moto pindi yanapotokea katika maeneo yao.

Waziri Mkuu amesema licha ya jeshi hilo kutoa elimu, pia wanatakiwa kuwashawishi wakazi wa maeneo ya mabondeni kuondoka kabla ya kutokea kwa maafa badala ya kusubiri majanga yatokee. Pia aliwataka wawe na mpango wa kuonesha eneo lenye maafa na kuujulisha umma.