Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli na Mke wake Mama Janet Magufuli wakiongoza waombolezaji Jijini Dar es salaam kuuga mwili wa Marehemu Christina Ghalima Lissu Mughwai.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli na mke wake Mama Janet Magufuli wamewaongoza wakazi wa jiji la Dar es salaam kuuaga mwili wa marehemu Christina Ghalima Lissu Mughwai ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu katika bunge la 10 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kutoka mkoa wa Singida.
Akisoma wasifu wa marehemu kaka wa marehemu Mheshimiwa Tundu Lissu amesema Marehemu aliyezaliwa 21.06.2016 na alifariki 07.04.2016 alikua ni nguzo muhimu kwa familia yao na tangu utoto wake alikuwa anasumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya kudumu pamoja na kifua kikuu.
Kwa upande wake mwakilishi wa serikali Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI nchini George Simbachawene amesema serikali imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya msiba huo kwa kuwa marehemu alikuwa akiwatumikia kwa uaminifu wananchi wake na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano wake.
Kiongozi wa kambi ya upinzani Freeman Mbowe amesema marehemu alikuwa na mchango mkubwa ndani na nje ya chama.
Kwa upande wake Naibu Spika wa bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson Mwansasu amesema ofisi ya bunge inatambua vyema mchango wa Marehemu Christina.
Marehemu alifariki siku ya Alhamis katika hospitali ya Agha Khan Jijini Dar es salaam akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani tangu mwaka jana na ameacha mtoto wa kike mmoja na mazishi yatafanyika kesho kijijini Mahambe mkoani Singida.









