Monday , 1st Jan , 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kufuatia vifo takribani 36 vilivyotokana na ajali  Dec 31 2017 katika barabara ya Nakuru - Eldoret nchini Kenya.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu imesema kwamba msiba huo umesababisha majonz makubwa kwani haushii Kenya tu na kwamba ni Jumuiya ya Afrika  Mashariki kwa ujumla.

"Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa ajali iliyosababisha ndugu zetu takribani 36 kupoteza maisha baada ya basi la abiria kugongana na lori katika barabara ya Nakuru - Eldoret nchini Kenya. Msiba huu umesababisha majonzi makubwa sio tu kwa ndugu zetu wa Kenya bali pia kwetu sote wana Jumuiya ya Afrika Mashariki, tumepoteza wapendwa wetu na nguvu kazi yetu" Imeeleza taarifa hiyo.

Imeongeza kuwa "Kwa niaba ya Watanzania wote nakupa pole sana ndugu yangu Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya kwa msiba huu mkubwa ulioupata, nawapa pole wana familia wote waliowapoteza jamaa zao na pia nawapa pole wananchi wote wa Kenya. Naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, nawaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka na Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina".