Tuesday , 3rd Nov , 2015

Watu wawili wamefariki dunia kutokana na kukumbwa na mafuriko ya mvua kubwa iliyonyesha kwa masaa kadhaa jijini Mwanza, akiwamo mwanafunzi wa kidato cha nne aliyesombwa na maji wakati akiwahi kufanya mitihani ya mwisho.

Uwanja wa ndege wa Mwanza ukiwa umefurika majii baada ya mvua kubwa kunyesha.

Mvua hiyo iliyoanza kunyesha saa 12 asubuhi, ilikatika saa 4:30 asubuhi na kusababisha baadhi ya barabara kuziba kutokana na maji kuporomoka kutoka milimani.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo ingawa hadi wakati anatoa taarifa hizo, mwili mwanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari Nyamanoro, ulikuwa haujapatikana.

“Mvua kubwa ilinyesha kwa masaa manne katika maeneo mbalimbali ya jiji iliyosababisha maporomoko kutoka milimani na kusababisha watu kukosa sehemu ya kupita hasa eneo la Kirumba ambako mwendesha bodaboda namba MC861 AHK aliyewapakiza wanafunzi wawili wa kidato cha nne, kusombwa na maji na dereva huyo kufariki lakini wanafunzi wakiokolewa,” alisema Mkumbo.

Kamanda Mkumbo amemtaja mwanafunzi wa shule ya sekondari Nyamanoro ambaye mwili wake haujapatikana ni, Zainabu Shabani (18) aliyekuwa na wenzake wawili waliokuwa wakivuka daraja llilopo maeneo ya Nyamanoro wilaya ya Ilemela.

“Wenzake walifanikiwa kuvuka daraja salama, lakini Zainabu hakumaliza safari yake na kusombwa na maji mpaka na sasa hajulikani kama amekufa ama yupo hai kutokana na mwili wake kutoonekana,” alisema.

Mkumbo aliwataka wananchi kuacha tabia ya kuvuka mitaro na maeneo yaliyojaa maji pindi wanapoona mvua kubwa inanyesha ili kuepuka vifo na mataizo yanayoweza kuepukika.

Katika hatua nyingine Meneja wa uwanja wa ndege wa Mwanza, Ester Madale, amesema wamelazimika kufunga kwa muda uwanja wa ndege wa mwanza baada ya maji kujaa kwenye njia za kurukia ndege.

Amesema sababu ya kufanya hivyo ni mvua iliyoanza kunyesha asubuhi na maji kuporomoka katika vilima ambavyo vimezunguka uwanja huo.

Naye meneja wa mamlaka ya hali ya hewa Kanda ya ziwa, Agustine Nduganda, amesema kunyesha kwa mvua hizo kumetokana na utabiri uliofanywa tangu mwezi Septemba mwaka huu.

Amesema kuwa juzi mamlaka yake ilitoa tahadhari kuhusiana na mvua hizo zilizonyesha mapema jana asubuhi.