Friday , 5th Dec , 2014

Taharuki kubwa imewapata wananchi wa kijiji cha Mabamba katika wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma baada ya mabomu manane ya kutupwa kwa mkono kufukuliwa  yakiwa yamehifadhiwa ardhini  karibu na  nyumba moja kijijini hapo.

Yanavyoonekana baadhi ya mabomu baada ya kufukuliwa

Taharuki kubwa imewapata wananchi wa kijiji cha Mabamba katika wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma baada ya mabomu manane ya kutupwa kwa mkono kufukuliwa  yakiwa yamehifadhiwa ardhini  karibu na  nyumba moja kijijini hapo.
 
Mabomu hayo yamegunduliwa na wachimbaji wa mtaro kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mganga katika  kituo cha afya Mabamba, ambapo mashuhuda wamesema wakati wakiendelea na uchimbaji wa mtaro walioyaona mabomu hayo na baada ya kutilia shaka walitoa taarifa kwa viongozi wao ambao  walifika na kuzuia wananchi waliokuwa wanasogelea eneo hilo bila ya tahadhari.
 
Mkuu wa wilaya ya kibondo Venance Mwamoto akizungumza na wananchi baada ya kufika katika kijiji hicho ambacho kipo katika mpaka wa Tanzania na Burundi amewataka wananchi kuchukua tahadhari wanapoona vitu wasivyovifahamu na kwamba serikali itafanya uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini yalifikaje katika eneo hilo ambalo lilikuwa likimilikiwa na diwani wa kata ya Mabamba Ali Gwanko
 
Kwa upande wake mtaalam wa mabomu kutoka JWTZ kikosi kiteule katika vijiji vya mpakani wilayani humo Damas Nyiitambe  ambaye alifanya kazi ya kuyategua mabomu hayo na kuyaweka katika usalama, pamoja na kutoa tahadhari kwa wananchi wanaopenda kukimbilia sehemu za hatari, amesema mabomu hayo ya kutupwa kwa mkono yametengezwa nchini china na urusi.