
Zitto Kabwe (katikati) akitoka Mahakamani
Taarifa za kufikishwa kwake mahakamani zilianza kusambazwa na Mke wake kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter ambao anatumia jina la Bwana Anna ambapo aliandika Mbunge huyo anapandishwa kizimbani ikiwa ni majira ya saa saba nusu mchana.
Katika Shauri hilo kwa mujibu upande wa Jamhuri wamewasilisha makosa matatu ya uchochezi kwa kiongozi huyo ambayo anadaiwa kufanya uchochezi akiwa jijini Dar es salaam kupitia mkutano wake na waandishi wa habari.
Aidha katika shauri hilo mahakamani upande wa Jamhuri uliwasilisha maombi ya kutopewa dhamana kwa mwanasiasa huyo kwa madai ya kulinda usalama wake.
Lakini kupitia upande wa Wakili wa Zitto Kabwe, Petter Kibatala uliwasilisha maombi ya kupatiwa dhamana kwa mteja wake kwa madai ya kuwepo kwa kasoro kwenye hati iliyowasilishwa na upande wa Jamhuri.
Hatimaye, Mahakama ikatupilia mbali maombi ya upande wa Jamhuri kwa madai ya kunyimwa dhamana kwa kiongozi huyo yalikuwa hayana mashiko na kuamuru Zitto Kabwe apewe dhamana kwa masharti ya saini ya mtu mmoja mwenye bondi ya shilingi milioni 10.