Friday , 17th Jul , 2015

Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde amelalamikia kuchezewa rafu na ofisi ya CCM Wilaya ya Chamwino kwa kuwaruhusu baadhi ya wanachama waliochukua fomu kuanza kufanya kampeni kabla ya muda.

Aliyekuwa mbunge wa jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde

Lusinde ametoa lawama hizo jana mbele ya waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu za kuwania ubunge kwa awamu ya pili katika jimbo la Mtera.

Amesema kanuni za CCM zinajulikana lakini kwa makusudi ofisi hiyo imemruhusu Samweli Malecela ambaye ni mtoto wa waziri mkuu mstaafu, John Malecela kuanza kampeni za uchaguzi tangu juzi huku wakijua kuwa ni kinyume na kanuni za chama hicho.

Amesema wapo wanachama wengi ambao wamechukua fomu tangu jana lakini wote wamezuiwa kuanza kampeni isipokuwa kwa mtoto huyo wa Malecela.

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Anthony Mavunde amechukua fomu ya kuwania kiti cha ubunge kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Dodoma mjini.

Mavunde ambaye kitaaluma ni mwanasheria amejitokeza kuwania jimbo hilo huku mbunge aliyemaliza muda wake naye pia ameshachukua fomu ya kutetea nafasi yake.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu kwenye ofisi za CCM Wilaya ya Dodoma mjini, Mavunde alisema kuwa amejipima na ana uhakika kuwa anaiweza nafasi hiyo na kuwaomba wananchi wa Jimbo hilo wamchague ili awatumikie.

Mpaka mchana wa leo jumla ya wagombea saba kutoka jimbo la Mtera walikuwa wamechukua fomu za kuwania ubunge huku kwa jimbo la Dodoma Mjini waliochukua fomu ni wanachama watano.

Huku katika Jimbo la Chilolwa kuna jumla ya wagombea 12 ambao wamejitokeza kuwania ubunge katika jimbo hilo .