Thursday , 4th Apr , 2019

Baada ya kusimamishwa kuhudhuria mikutano mitatu ya Bunge, Mbunge wa Arusha Mjini, Godblless Lema amesema kwamba moyo wake kwa sasa una amani kwani mahusiano yake na haki yanazidi kuimarika.

Godbless Jonathan Lema

Lema ameandika ujumbe huo muda mfupi baada ya Bunge kutoa maamuzi ikiwa ni siku moja baada ya Kamati ya Maadili kumhoji kwa kuunga mkono kauli ya CAG kwamba Bunge ni dhaifu.

Lema anakuwa ni Mbunge wa pili wa CHADEMA, kusimamishwa kuhudhuria vikao vya bunge kwa kuunga mkono kauli ya CAG iliyotafsiriwa kwamba ililenga kulidhalilisha bunge, Halima Mdee wa Kawe naye amesimamishwa kuhuduria Mikutano miwili.

"Nimesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge mpaka January 2020. Moyo wangu una amani sana, kwani mahusiano yangu na haki yanaendelea kuimarika zaidi. Nawatakia Wabunge wenzangu kazi njema katika wajibu huu, sitanyamaza hata kama adhabu itakuwa ni mauti" Lema.

Hukumu ya Lema na Halima, imetokea ikiwa ni baada ya April 2, 2019, Bunge la Tanzania kuazimia kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali CAG, Prof Mussa Assad kwa kutoa kauli iliyoashiria kulidhalilisha Bunge baada ya kusema kuwa Bunge ni 'dhaifu'.