Waziri wa Uchukuzi na mbunge wa Kyela akitembelea baadhi ya maeneo yaliyothirika na mafuriko Wilayani Kyela
Waziri wa uchukuzi mheshimiwa Dkt Harrison Mwakyembe amesema kuwa wananchi wa wilaya ya Kyela wameathiriwa kwa kiwango kikubwa kutokana na mafuriko yaliyotokea mwaka huu na kwamba misaada ya haraka inahitajika ili kuhakikisha havitokei vifo vya watu wengine kutokana na mafuriko hayo.
Dkt. Mwakyembe ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kyela amesema hayo wakati alipotembelea wananchi waliokumbwa na maafa hayo na kutoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu zao.
Amesema kata 12 zimepata mafuriko makubwa na baadhi ya vijiji ndani ya kata hizo vimekuwa kama visiwa na hakuna mawasiliano ya barabara, madaraja na hata miundombinu mingine imeharibiwa.
Baadhi ya viongozi wa kata zilizohathiriwa na mafuriko hayo wamesema idadi kubwa ya wananchi wamepoteza chakula nyumba, makazi, mazao pamoja na mashamba kufutia baadhi ya mito mikubwa kuhama njia.
Wamesema kuwa wananchi hao mpaka sasa wanaendelea kuishi kwa ndugu, majirani na katika taasisi kama shule na makanisa na wanahitaji msaada wa haraka wa chakula mavazi.
Ni wiki tatu tangu kutokea kwa mafuriko hayo ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu watano na wengine kunusurika na mpaka sasa baadhi ya huduma muhimu za kijamii bado hazijarejea katika hali ya kawaida.
Wanafunzi wengine wameendelea kubaki nyumbani maana hakuna hata barabara na shule nyingine madarasa yake yamebomoka na vyoo vyote vimesombwa na maji.