Thursday , 31st Mar , 2016

Kamati ya Bunge Mitaji na Uwekezaji imelitaka Shirika la Nyumba la Taifa NHC kuhakikisha inashusha bei za ununuzi wa nyumba ili wananchi wa kipato cha chini waweze kuwa miongoni mwa wamiliki wa nyumba zinazojengwa na shirika hilo.

Wakiongea katika majadiliano ya kamati hiyo wabunge wamesema kuwa shirika hilo limekuwa likitaja bei nafuu lakini kiuhalisia bei sio nafuu.

Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo ndugu Nehemia Mchechu amefafanua kuwa ni vigumu kuuza nyumba kwa bei ya chini ikizingatiwa kuwa upatikanaji wa ardhi na gharama za ujenzi ziko juu hivyo kuitaka serikali kupunguzia kodi shirika hilo ili iweze kuuza nyumba kwa garama nafuu.

Aidha, Nehemia Mchechu ameitaka kamati hiyo kuishauri serikali kuwekeza zaidi katika sekta ya nyumba ili kuweza kumudu mahitaji ya wananchi wake katika miaka ijayo kwani inakadiriwa kuwa ifikapo 2025 Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zenye watu wengi zaidi duniani hivyo ni vyema kuwa na mikakati endelevu ya makazi bora.

Mchechu pia amewataka wabunge kuishinikiza serikali kutengeneza sera ya sekta ya nyumba kuliko ilivyo hivi sasa ambapo sekta hiyo haijapewa kipaumbele licha ya kuwa na manufaa makubwa ya kiuchumi kwani sekta ya ujenzi hutengeneza nafasi nyingi za ajira.