
Kubenea ametoa kauli hiyo ikiwa yupo katika muendelezo wa kumuombea ridhaa mgombea Ubunge wa jimbo la Kinondoni kupitia (CHADEMA), Salum Mwalimu ili aweze kupigiwa kura ya ndio kwa wingi na wananchi wa jimbo hilo na aweze kukalia kiti hicho ambacho kwa sasa lipo wazi kutokana na Mbunge wa awali Maulid Mtulia kujivua uachama wake na nafasi nyingine zote alizokuwa nazo katika chama chake cha CUF.
"Katika uchaguzi huu kama kuna michezo waliyocheza huko nyuma hapa ndio mwisho. Nimejiandaa kwa jua na mvua, giza na nuru lakini tutahakikisha kura zenu mtakazopiga zinahesabiwa. Tunajua mipango iliyopangwa na vigogo watatu wakubwa wa CCM wa kuhujumu uchaguzi huu tunafahamu na tunataka kuwahakikisha kwamba hawatafanikiwa", amesema Kubenea.
Pamoja na hayo, Kubenea ameendelea kwa kusema "tumejipanga kikamilifu na tulipoingia katika uchaguzi huu wa marudio tumejiandaa kwa kila kitu, kwa hiyo tunawaahidi wananchi mkapige kura ila kazi ya kulinda kura zenu tutazifanya kwa nguvu zote".
Kwa upande mwingine, Kubenea amewahakikishia wananchi kwamba Salum Mwalimu ni mtu aliyekuwa safi kwa madai kipindi alipokuwa mwanahabari katika chombo kimoja wapo kilichopo jijini Dar es Salaam aliweza kutetea maslahi ya taifa hivyo akipewa ridhaa ataweza kuwatendea haki wanakinondoni vizuri.