Friday , 26th Oct , 2018

Mwanafunzi Ndemezo Rutakwa ambaye ameshika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka 2018, amesema Kiingereza cha kuandika ni kigumu kuliko cha kuongea.

Mwanafunzi Ndemezo Rutakwa akiwa amebebwa baada ya matokeo kutangazwa.

Akiongea na MJADALA wa East Africa Television leo kwa njia ya simu kutoka kwao Chato mkoani Geita, Ndemezo amesema yeye binafsi anaamini kuongea Kiingereza ni rahisi kuliko kukiandika.

''Kiingereza kwenye shule yetu ni somo rahisi tu kwasababu ndio lugha tunayotumia lakini inahitaji kukizoea kwanza pia kukiongea kila wakati haijalishi upo mazingira ya shule au nyumbani maana hiyo inarahisisha kukizoea na kukiandika vizuri maana kuongea ni rahisi kuliko kuandika'', amesema.

Ndemezo ambaye ni mhitimu katika Shule ya Msingi Kadama English Medium iliyopo Kata ya Buseresere wilayani Chato, ameeleza kuwa wanafunzi wengi wageni walikuwa wanapata taabu wakifika shuleni hapo lakini wakizoea waliona somo hilo ni la kawaida.

Aidha Ndemezo amesisitiza kuwa Kiingereza kinakuwa kigumu kwa shule ambazo hazitumii lugha hiyo kama lugha rasmi ya shule hivyo ikiwezekana shule ziwe na utaratibu huo kwani unasaidia wanafunzi kukizoea na kufaulu somo hilo.