Thursday , 9th Oct , 2014

Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amewapongeza wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa kupendekeza katiba ambayo imejali maslahi ya makundi yote wakiwemo wanawake na walemavu.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Ally Mohammed Shein, wakifungua katiba inayopendekezwa.

Rais Kikwete amesema hayo Oktoba 8, 2014 mjini Dodoma wakati alipokuwa akikabidhiwa katiba iliyopendekezwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba mara baada ya kumalizika kwa vikao vya bunge hilo maalum la katiba.

Kwa upande wake Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein amesifu namna Zanzibar ilivyoshirikishwa ipasavyo katika kila hatua ya mchakato huo na kusema kwamba sasa wana jukumu la kuweka utaratibu maalum ili waweze kuipigia kura katiba hiyo inayopendekezwa.

Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya uandishi, Andrew Chenge alisema katiba hiyo imejali maslahi ya wote na imetokana na Rasimu ya pili ya katiba iliyowasilshwa katika Bunge Maalumu la Katiba ili kuijadiliwa na kuiboresha.