Thursday , 18th Feb , 2016

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi prof. Makame Mbarawa amewataka wafanyakazi wote wa wizara yake mkoani Simiyu kuwa waadilifu na atakayeshindwa kufanya hivyo ataoneshwa mlango wa kutokea kwa kupewa kilicho chake ili kupisha wanaohitaji.

Waziri wa ujenzi ,mawasiliano na uchukuzi prof. Makame Mbarawa

Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani Simiyu ya kukagua barabara ya Lamadi hadi Bariadi yenye kilomita 71 ambayo iko katika hatua za mwisho kukamilika na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Mwigumbi Shinyanga hadi Maswa yenye kilomita 50.3 pindi alipokutana na wafanyakazi wote walioko katika wizara yake

Waziri amesema kuwa uadilifu katika sekta ya miundombinu ni muhimu katika kuchochea kasi ya maendeleo na hatimaye Tanzania kuingia katika uchumi wa kati, hivyo ni vema wafanye kazi kwa bidii na ubunifu sambamba na kujiepusha na vitendo vya rushwa.

Akiwa katika kambi ya kampuni ya Chicco inayojenga barabara ya Mwigumbi Maswa amemtaka mkandarasi kufanya kazi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango kizuri na akifanya kwa kiwango cha chini hatasita kumuondoa na kumtafuta mkandarasi mwingine.

Aidha alitoa onyo kwa wafanyakazi wa sekta ya mawasiliano kutojihusisha kuwa madalali wa makampuni mengine, huku akitolea mfano kampuni ya TTCL na endapo akisikia mtu anajihusisha na hilo lazima atamuondoa kazini.

Wakati huo huo Waziri Mbarawa, amezitaka halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu kukusanya kodi ipasavyo kwa kutumia mtandao wa elekroniki na kuachana na mfumo wa zamani wa kutoa risiti za karatasi.

Mhe. Mbarawa amesema hayo katika ziara yake ya siku moja Mkoani Geita ambapo amesema kuwa serikali imeamua kusisitiza mfumo huo wa ukusanyaji wa kodi ili kuepukana na mianya ya Rushwa.

Waziri huyo ameongeza kuwa serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano ili kuweza kufanikisha suala hilo la ukusanyaji wa kodi kwa ufanisi na kuweza kuliongezea taifa pato.

Mhe. Mbarawa ameongeza kuwa kwa sasa hakutakua na mtindo wa kufikishiana pesa mkononi na kukatiwa risiti kwa kuwa mafumo huo unaoyesha unatumika kuikosesha mapato serikali kwa watumishi wasio waaminifu.