Rais Magufuli akifurahi pamoja na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad mara baada ya kupokea ripoti hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Ametoa agizo hilo leo wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Ripoti hiyo imewasilishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Prof. Mussa Juma Assad katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
“Haiwezekani Watanzania wanakosa dawa hospitali wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa maji wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa umeme wakati dhahabu zao zinaondoka, Watanzania wanakosa barabara wakati dhahabu zao zinaondoka, nataka ukakague kwa kina hii sekta ya madini ili watanzania wajue chao nini na kama kinapatikana sawasawa?” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Rais Magufuli akizungumza mara baada ya kupokea Ripoti hiyo ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad Ikulu jijini Dar es Salaam.
Mhe. Dkt. Magufuli pia amemuagiza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kuitisha kikao cha pamoja kitakachomkutanisha CAG na Mawaziri wote, Makatibu Wakuu wa wizara zote, Gavana wa Benki Kuu na Wakuu wa taasisi za umma ili kila mmoja aambiwe hali ya hesabu katika taasisi yake na kuchukua hatua.
“Mhe. Waziri Mkuu ukaongoze hicho kikao na wewe CAG uwaambie kila mmoja katika eneo lake juu ya dosari zake, sitaki kuona dosari zinajirudia zilezile kila wakati” amefafanua Mhe. Rais Magufuli.
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad akizungumza kabla ya kuwasilisha Ripoti hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam
Ripoti hiyo imegusa maeneo mbalimbali yakiwemo ukaguzi wa hali ya hesabu za Serikali, misamaha ya kodi, ukusanyaji wa kodi na maduhuli ya Serikali, uandaaji na utekelezaji wa bajeti, hali ya deni la Taifa, usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa mali na madeni ya Serikali na usimamizi na uendeshaji wa taasisi za umma zikiwemo taasisi muhimu za kifedha na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Prof. Mussa Juma Assad amesema pamoja na hatua kubwa iliyopigwa na Serikali katika kuzingatia taratibu za fedha bado kuna mapungufu mbalimbali ambayo yameendelea kujitokeza na ameshauri hatua zichukuliwe kukabiliana nayo ikiwemo kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma katika madini, kuiepusha TANESCO kununua umeme wa gharama kubwa, matumizi mabaya ya misamaha ya kodi na kuongeza mashine za kutoa risiti (EFD).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad mara baada ya kupokea ripoti hiyo Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, CAG anapaswa kuwasilisha ripoti ya hesabu za Serikali kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya tarehe 31 Machi ya kila mwaka, na baada ya hapo ripoti hiyo huwasilishwa bungeni katika kikao kinachofuata.
