Tuesday , 2nd Feb , 2016

Mbunge wa jimbo la Kigoma mjini Zitto Zuberi Kabwe, ameitaka serikali na bunge kupitisha uamuzi kuhusu kuongeza vyo vya ufundi stadi hapa nchini, kwa kuyatoa mafunzo hayo kwenye kambi za JKT.

Zitto kabwe ametoa wito huo leo alipokuwa akichangia hoja bungeni mjini Dodoma, na kusema kuwa vyuo vya ufundi vimekuwa vichache, hivyo kupelekea kuwa na vijana wachache wenye taaluma ya ufundi stadi.

“Tupendekeze kuwepo kwa VETA na technical college, tunahitaji mafundi wa kuwasaidia wahandisi, bila kuwa na veta za kutosha hatutakuwa na mafundi, mapendekezo ni kwamba naomba wabunge tukubaliane kuanzia sasa kila kambi ya JKT iwe na chuo cha VETA, wanaotoka JKT wawe na mafunzo wanapoenda mtaani waweze kupata ajira”, alisema Zitto Kabwe.

Pamoja na hayo Zitto Kabwe amesema hivi sasa mikoa mingi ambayo ilikuwa na vyuo vya ufundi akitolea Dar Tech na Arusha Tech, vyuo hivyo vimekufa na kubadilishwa matumizi yake, hivyo wakati umefika kwa serikali kuvifufua na kuongeza vingine mikoani, angalau kwa kila mkoa kuwe na chuo kimoja cha ufundi.

"Angalau kila mkoa uwe na technical school, kulikuwa na vyuo zamani Dar, Arusha tech, vyuo vya ufundi vimegeuzwa kuwa vyuo vikuu, kwa kuanzia tuanzie na vyuo vya JKT", alisema Zitto Kabwe.

Pia Zitto Kabwe ameitaka serikali kuruhusu mashirika hodhi kuwa na hisa kwenye shirika la ndege nchini ATCL ili yaweze kusaidia shirika hilo kujiedesha, na si kukimbilia kununua ndege mpya ili kutatua tatizo linaloikabili shirika hilo.

"Ununuzi wa ndege wa shirika la ndege, haiwezi serikali kila wakati iwe inanunua ndege, kuna watu ambao wanafaidika kwa kuwepo kwa shirika la ndege, nazungumzia mashirika ya utalii kama TANAPA, kutokana na wigo wa utalii wanapata mapato turuhusu wawe na hisa ndani ya ATCL ili shirikka liweze kujiendesha, ili mashirika yenye ukwasi yaweze kusaidia mashirika ambayo yako chini", alisema Zitto kabwe bungeni mjini Dodoma.