Rais Kikwete na Rais Goodluck Jonathan wakiwa kwenye moja ya vikao vya mkutano wa Uchumi kwa bara la Afrika nchini Nigeria
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Alhamisi, Mei 8, 2014, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Nigeria, Mheshimiwa Goodluck Jonathan katika Hoteli ya Transcorp Hilton katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Abuja.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete kwa mara nyingine, amewasilisha rambirambi rasmi za Tanzania, za Watanzania na za kwake mwenyewe kwa kiongozi huyo wa Nigeria kufuatia vitendo vya kigaidi ambavyo vimeua maelfu ya watu na wengine kutekwa nyara katika maeneo mbali ya nchi hiyo na hasa kaskazini.
Rais Kikwete pia ametoa pongezi nyingi kwa Rais Jonathan na wananchi wa Nigeria kwa kuandaa Kongamano la Uchumi Duniani (WEF-Afrika) kwa Afrika lenye mafanikio makubwa. Kongamano hilo lilianza jana na linamalizika kesho mjini Abuja na Rais Kikwete amejiunga na viongozi kadhaa duniani kuhudhuria Kongamano hilo.
“Mheshimiwa Rais, nakushukuru sana kwa kupata muda wa kuja kujiunga nasi katika mkutano wetu huu mkubwa. Kama ulivyosema wewe mwenyewe kuwepo kwako na kwa viongozi wengine ni ishara muhimu kwa dunia kuwa nchi yetu, pamoja na matatizo makubwa ambayo tunapitia, bado inaungwa mkono duniani na ina usalama wa kutosha kuweza kuendesha mkutano kama huu,” Rais Jonathan amemwambia Rais Kikwete.
Naye Rais Kikwete amemwambia Rais Jonathan: “Tunakupogeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuandaa kongamano zuri hapa nchini kwako. Kama unavyojua miaka yote makongamano hayo yalikuwa yanafanyika mjini Cape Town, Afrika Kusini, mpaka sisi Tanzania tulipoandaa Kongamano la kwanza nje ya Afrika Kusini. Siyo kazi rahisi, tunakupongeza sana.”
“Na yale yanayoendelea katika nchi ni uendawazimu wa kiwango cha juu sana – binadamu anao uwezo mkubwa sana wa kufanya mambo ya ukatili wa hatari kabisa. Hawa ni watu wasio na roho wala moyo. Ni ukatili wa kiwango cha juu sana,” amesema Rais Kikwete.
Hata hivyo, Rais Jonathan ameonyesha matumaini kuwa ugaidi huo unaweza kuwa unaelekea mwisho hasa kufuatia uamuzi wa Marekani na Uingereza kuisaidia Nigeria kukabiliana na hali hiyo. Ufaransa na China pia zimejitolea kusaidiai.
Moja ya mambo yanayoiwekea shinikizo Serikali ya Rais Jonathan kwa sasa ni kutekwa nyara kwa watoto wa kike wa Sekondari zaidi ya 200 katika shule moja kaskazini mwa nchi hiyo zaidi ya wiki tatu zilizopita. Mpaka sasa hawajulikana walipo na kikundi cha Boko Haram ambacho kinapinga elimu ya magharibi kimesema kinawashikilia watoto hao na kinataka kuwauza kwenye utumwa.
Juzi, Kikundi hicho ambacho kinafanya kila aina ya ugaidi kiliteka nyara watu wengine wanane kutoka kijiji kimoja cha kaskazini mwa nchi hiyo na usiku wa jana, kikundi hiki kilivamia vijiji kadhaa na kuua watu zaidi ya 300.