Monday , 2nd May , 2016

Halmashauri ya jiji la Dar es salaam, imeendelea kushinikiza msimamo wake wa kutiuza asilimia 51

Halmashauri ya jiji la Dar es salaam, imeendelea kushinikiza msimamo wake wa kutiuza asilimia 51 ya umiliki wa hisa zake kwenye shirika la UDA na kwamba hakuna nyaraka zozote zinazoonyesha uhalali wa mauzo hayo.

Akiongea na East Africa Radio wakati wa uwasilishwaji wa taarifa za kamati zilizoundwa kuchunguza mali zinazomilikiwa na Jiji, mjumbe wa baraza la halmashauri ya jiji na Meya wa manispaa ya kinondoni Diwani Boniface Jackob amesema, UDA haikuuzwa bali ni mchakato wa kitapeli hivyo wao kama baraza watashikilia msimamo kuwa Simon Group hana nyaraka zozote za mauzo ya hisa hizo.

Jackob amedai kuwa, Taarifa iliyotolewa na Msajili wa hazina kwa vyombo vya habari hivi karibuni kuwa UDA tayari imemaliza malipo ya hisa zake kwa jiji na kuainisha kuwa fedha zilioingia bila taarifa hawaitambui na kumtaka Rais kumchunguza msajili wa hazina kwani hawezi kutunza mali za serikali kulingana na utendaji wake kuwa na mashaka , akigusia zaidi mgongano wa kauli zake juu ya sakata hilo na ule wa CAG aliouonyesha.

Jackob amesema, licha ya kuwa meya wa jiji la Dar es salaam, hajakabidhiwa ofisi na Meya aliye maliza muda wake wao kama wajumbe wataendelea kushinikiza kufanyika upya kwa usajili wa mikataba yote ya mali za jiji, ikiwemo viwanja, maeneo ya maduka, majengo, mashirika pamoja na kuweka malipo yanayoendana na wakati na kuongeza kuwa mchakato huo utawapa fursa ya kuwatambuwa wamiliki wote na vitega uchumi vya jiji.