Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la nchini Japan – JICA, leo limesaini makubaliano na Wizara ya Fedha na Mipango ambapo lishirika hilo litaipatia serikali ya Tanzania mkopo wa shilingi bilioni 210 kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 508 za njia ya umeme utakaoziunganisha Tanzania na Kenya.
Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, mwakilishi mkazi wa JICA nchini Bw. Toshio Nagase amesema Tanzania ndiyo itakayofaidika zaidi na fedha hizo kwani kati ya kilomita 508 za umeme zitakazojengwa, kilomita 415 zipo nchini Tanzania na 93 zilizobakia zipo nchini Kenya.
Kwa mujibu wa Bw. Nagase, mradi huo unatarajia kukamilika ifikapo mwaka 2019 na kwamba mara utakapokamilika, utachochea kasi ya ukuaji wa uchumi kwani Tanzania na Kenya zitakuwa na nishati ya uhakika kwa ajili ya uzalishaji mali.