Thursday , 3rd Mar , 2016

Jamii wilayani Mbozi mkoani Songwe imetakiwa kutobweteka na Sera ya serikali ya Elimu bure badala yake itumie fursa hiyo kama chachu ya kuelekeza nguvu yake kwenye changamotozinazoikabili sekta hiyo ikiwemo ujenzi wa shule mpya na kuongeza madarasa.

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Ilolo wilayani Mbozi wakiwa katika paredi wakati wa kupandisha bendera ya taifa

Changamoto ya uhaba wa Vyumba vya madarasa na shule kwa ujumla imeibuka katika maeneo mbalimbali wilayani hapa baada ya wazazi na walezi kuhamasika kuandikisha watoto wengi kuanza shule yakiwa ni matokeo ya sera ya Elimu Bure.

Ofisa Elimu taaluma wilayani Mbozi,Samweli Mshana amesema ni wakati kwa jamii sasa kuelekeza nguvu zote kukabiliana na matokeo ya sera ya Elimu Bure badala ya kubaki ikipiga porojo za kusifia sera hiyo inayoishia kwa kuboresha maisha ya mwanafunzi aliye darasani tayari.

Mshana ametoa kauli hiyo katika maeneo na nyakati tofauti katika vijiji vya Lumbila, Igale, Iyula B na Ilomba, alipoambatana na Mbunge wa jimbo la Vwawa Japheti Hasunga kukabidhi misaada ya mabati na saruji katika sekta ya elimu na afya ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kusukuma maendeleo kwenye jimbo hilo.

Amesema jamii inaweza kutafsiri vibaya sera ya elimu bure ikaacha kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa na miundombinu mingine ,matokeo yake likazalishwa tatizo lingine kubwa la ukosefu wa vyumba hivyo ambalo serikali itashindwa kulitatua mara moja,

Ameongeza kuwa iwapo wananchi wataendelea kujenga vyumba vya madarasa na ujenzi wa shule mpya,ongezeko la uandikishaji wanafunzi litakwenda sambamba na,miumdombinu iliyopo.

Kwa upande wake Mbunge wa Hasunga akikabidhi michango yake katika vijiji hivyo ambayo ni mifuko 100 ya saruji, mbao 30, fedha tasilimu Sh. 300,000 kwa ajili ya kikundi cha wanawake wajane na bati 30 vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh. 2.5 Milioni, amesema kuwa atakuwa tayari kuchangia shughuli za maendeleo ili kuwatia nguvu wananchi popote katika jimbo hilo.