Wednesday , 17th Jun , 2015

Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani mchana wa leo amechukua fomu ya kuomba kuwania urais waTanzania kwa tiketi ya CCM

Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Augustino Ramadhani leo amechukua fomu ya kuwania urais kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema kuwa kama atafanikiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atakabiliana na vitendo vya rushwa na ufisadi kwa mujibu wa sheria za kukabiliana na rushwa zilizopo nchini.

Aliwasili makao makuu ya CCM majira ya saa sita na nusu akisindikizwa na familia yake pekee na mara baada ya kuchukua fomu akifanya mkutano na waandishi wa habari na kueleza mambo mbalimbali yaliyomsukuma kuwania nafasi hiyo.

Jaji Ramadhani ambaye ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa CCM makao makuu mjini Dodoma.

Amesema kwa kipindi chote alichotumikia nchi katika nafasi mbalimbali hadi kufikia jaji mkuu hajawahi kutuhumiwa na mtu yeyote kupokea rushwa na hivyo atahakikisha kuwa anakabiliana nayo kwa mujibu wa sheria.

Kuhusu matukio ya kinyama na kikatili yakiwemo mauaji ya albino ambayo siku za hivi karibuni yameshika hatamu na kulitia taifa doa ulimwenguni jaji Agustino amesema mambo hayo yanahitaji ushirikiano wa hali ya juu kati ya jamii na mamlaka ikiwemo kutoa elimu ya kutosha kuondoa imani hizo huku akionya hatakuwa na mzaha kwa watu watakaobainika kuhusika.

Jaji Agustino Ramadhani anakuwa kada wa 36 wa chama cha mapinduzi CCM kuingia katika kinyang'anyiro cha kuwania urais kupitia chama hicho.

Amesema dhamira kubwa iliyomsukuma kugombea urais ni kwamba ana uwezo wa kuiongoza nchi kwa kuinua maisha ya watanzania walio wengi.