Monday , 22nd Dec , 2014

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, amesema mkoa wake utapata jengo la makumbusho la kisasa kabisa litakalokuza sekta ya utalii pamoja na kuwawezesha wajasiriamali wadogo na kuongeza ajira kwa jamii ya Iringa.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza.

Mkuu huyo wa mkoa amesema Nyanda za Juu Kusini licha ya kuwa na vivutio vingi vya utalii, hata hivyo bado rasilimali hiyo haijatumika ipasavyo ili kuweza kuchangia katika kukuza maisha ya jamii hii kutokana na kukosekana kwa ufahamu bora miongoni mwa wanajamii juu ya umuhimu wa wa urithi huu wa utamaduni na utalii kwa maendeleo ya sekta ya utalii na biashara.

Masenza amesema jengo hili la kisasa la makumbusho litakuwa katika iliyokuwa ikifahamika kama Iringa Boma, ambapo sasa litatumika kwa ajili ya kuonesha mambo ya urithi wa kihistoria na kuvutia watalii duniani kote kuja kutembelea Tanzania hasa mkoa wa Iringa.

Mkuu huyo wa mkoa amesema ajira nyingi zitaongezeka kuanzia ukarabari wa jengo hilo la zamani na vilevile wasomi wa taaluma ya makumbusho na uhifadhi wataajiriwa katika kuhudumia makumbusho haya ya kisasa.