Sunday , 21st Oct , 2018

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro amekanusha taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa amefanya mabadiliko katika baadhi ya mikoa na kuwashusha vyeo baadhi ya watendaji, akiwemo, Kamanda wa Kanda maalum ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro (kulia) na Kamanda wa Kanda maalum ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi hilo Barnabas Mwakalukwa imesema kuwa siku za hivi karibuni kumeibuka kikundi cha watu wachache kilichoamua kulichafua jeshi kwa kuchapisha taarifa za uongo.

"Serikali na vyombo vyake ina utaratibu zake za kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na mambo mbalimbali ikiwemo uhamisho na uteuzi wa maafisa wake", imesema taarifa hiyo.

Taarifa ya Mwakalukwa imesema kuwa IGP, Sirro amewataka wananchi kuzipuuzia taarifa hizo kwakile alichodai kuwa zinalengo la kupotosha, na tayari wameanza uchunguzi wa kuwabaini waliohusika na usambazaji wa taarifa hizo.

Mapema leo kupitia mitandao ya kijamii, zilisambaa taarifa zikidai kuwa IGP Simon Sirro amefanya mabadiliko ya kuhamisha na kuwashusha vyeo baadhi ya maafisa wa jeshi la polisi nchini akiwemo, Kamanda wa Kanda maalum ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa.