
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama
Waziri Mhagama ametaja baadhi ya vitendo vya ukatili ambavyo wanawake hukumbana navyo kuwa ni pamoja na kutopandishwa vyeo, kulipwa maslahi na ujira mdogo, kutokuajiriwa na kunyanyaswa au kudaiwa rushwa ya kingono ili wapate haki zao.
Akifungua kikao cha viongozi wanawake wa vyama vya wafanyakazi nchini na wale wa Chama cha Waajiri nchini (ATE) mjini Dodoma, Mhagama manyanyaso mengine ya wanawake sehemu za kazi ni kupoteza ajira pale wanapojifungua, kunyimwa kinga na likizo za uzazi, kunyimwa ruksa ya kunyonyesha n.k
Amesema vitendo hivyo ni vya kibaguzi ambavyo havikubaliki na vyenye madhara makubwa kwa wanawake kwa sababu vinawanyima fursa sawa katika ajira, hivyo kupelekea watumbukie kwenye lindi la umaskini na kuathiri mchango wa kukuza uchumi wa nchi.
“Sheria za kazi hususani sheria za ajira na mahusiano kazini namba 6 ya 2004, inaeleza ni marufuku kwa mwajiri kumbagua mfanyakazi katika masuala yahusuyo kazi na ajira kwa misingi ya jinsia, jinsi , ujauzito na majukumu ya kifamilia,” amesema Mhagama.
Hata hivyo, amesema nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwamo Tanzania, zilipitisha ajenda ya maendeleo endelevu 2030 yenye malengo 17, miongoni mwao ikiwa ni lengo Na. 5 linalohusu usawa wa kijinsia katika Nyanja zote za kiuchumi na kijamii.