Tuesday , 27th Jan , 2015

Serikali imeliagiza jeshi la polisi nchini kuwachukulia hatua kali za kisheria askari wake wote waliohusika katika kuwaonea wananchi wakati wa kuwakamata wahalifu wanaounda kundi la Panya Road.

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mathias Chikawe

Agizo hilo limetolewa jana mjini Dodoma na Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mathias Chikawe wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa maofisa waandamizi wa jeshi la polisi nchini.

Chikawe amesema kuwa wananchi wa Dar es Salaam wanalituhumu jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es salaam kuwa baada ya kuwakamata vijana wengi lilifanya mradi kwa kauli kuwa kuingia bure kutoka kwa pesa.

Kwa upande wake Inspekta Jeneral wa polisi (IGP) Ernest Mangu amesema nchi inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama ambapo katika mkutano huo watajadili na kujikosoa wapi wamekosea ili kuongeza jitihada za kuweza kukabiliana na uhalifu.

Hata hivyo alisema takwimu za uhalifu wa jinai za mwaka 2014 zinaonesha kushuka kwa vitendo hivyo kwa asilimia 5.7 ikilinganishwa na mwaka 2013 viliposhuka kwa asilimia 1.1 tu.