Monday , 27th Jul , 2015

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Mtwara hatimaye kimewapata wagombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini na wa viti maalum, baada ya kufanikiwa kukamilisha zoezi la uchaguzi ulioshindwa kufanyika Julai 22 mwaka huu.

Mgombea Ubunge kwa Tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Bw, Joel Nananuka

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika jana, mwenyekiti wa chama hicho kanda ya kusini, Namangaya Hamisi Namangaya, amemtangaza Joel Nanauka kuwa ndio kinara kwa kupata ushindi wa kishindo baada ya kuwazidi wapinzani wake kwa idadi kubwa ya kura.

Akizungumza baada ya kujua matokeo, Nanauka ambaye alianguka ghafla ukumbini wakati wa kujinadi kwa wajumbe baada ya kupewa dakika tano na kupoteza fahamu, amemshukuru mwenyezi mungu kwa matokeo yaliyotangazwa na anaamini wanachadema wamemchagua kiongozi waliemuhitaji.

Aidha Nanauka aliyezungumzia suala la kuanguka kwake na kusema kuwa kulitokana na presha pamoja na sukari kushuka kwa kiasi kikubwa lakini anashukuru Mungu anaendelea vizuri na yupo tayari kuipeperusha bendera ya CHADEMA katika jimbo hilo la Mtwara mjini.