Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.
Dk. Shein aliyasema hayo huko Tibirinzi Chake Chake Pemba, alipokwenda kukagua Tawi la CCM lililochomwa moto katika ziara yake ya kukagua athari zilizofanywa dhidi ya wanachama wa CCM kwa kuendelea kukiunga mkono chama hicho kiswani humo.
Katika maelezo yake, Dk. Shein aliwataka wananchi kutambua kuwa hapatakuwa na uchaguzi tena hapa Zanzibar hadi mwaka 2020 na kuwasisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ipo na itaendelea kuwepo.
Dk. Shein aliwataka wananchi kuyapuuza maneno hayo ya wapinzani kwani ni utani na dhihaka wanayoambiwa wananchi kuwa uchaguzi mkuu hapa Zanzibar utarejewa na kusema kuwa hilo halipo na hakuna hata taifa ama nchi inayoweza kuishurutisha Zanzibar kufanya uchaguzi.
Alisema kuwa Zanzibar inaongozwa kwa Katiba na Sheria za nchi, hivyo hakuna wa kuiongoza na kuleta matakwa yake ili yafuatwe na Zanzibar ili uchaguzi urejewe.
Dk. Shein alisema kuwa yeye amewekwa na wananchi kwa mujibu wa Sheria na Katiba ya nchi, hivyo maneno ya dhihaka na utani yanayopitwa yakisemwa na wapinzani kuwa uchaguzi utarejewa ni kasumba za kisiasa.
Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo na yeye ndie Rais na kamwe hujuma wanazofanyiwa wanaCCM kisiwani humo hazitoiondoa ama kuifanya isifanye kazi zake. "Wataumwa hadi kuvimba matumbo lakini mimi ndie Rais halali wa Zanzibar na nitaendelea kuiongoza Zanzibar hadi mwaka 2020 utakapoitishwa uchaguzi mwengine,” alisema Dk. Shein.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alisisitiza kuwa Serikali haipatikani kwa hujuma, vitimbi ama kufukiza udi, uvumba na ubani bali serikali hupatikana kwa kufuata misingi ya demokrasia na sheria za nchi kama ilivyofanya CCM na hatimaye kushika dola.
Dk. Shein aliwataka wananchi hao kutokuwa na hasira kwani chama chao cha CCM kimeshinda na ndicho kinachoongoza Serikali na yeyote mwenye nia ya kuvuruga amani na utulivu uliopo hapa nchini basi nguvu za dola zipo na zitapambana nao.
“Mimi nimewekwa kwa ridhaa za wananchi kwa mujibu wa sheria na Katiba na hata Mwenyezi Mungu anajua kuwa mimi ndie Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwani yeye ndie alieniwetaka na asingelitaka yeye nisiwe rais basi nisingelikuwa rais,” alisisitiza Dk. Shein.
Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi na wanaCCM kuendelea na kazi zao kama kawaida na kushirkiana na serikali kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo kwa kuamini kuwa Serikali yao ipo na itaendelea kushirikiana nao.
Nao WanaCCM wa Tawi hilo walieleza masikitiko yao juu ya hujuma walizofanyiwa za kutiliwa moto Tawi lao kwa makusudi jambo lililopelekea hasara ya zaidi ya Shilingi milioni 9 za Kitanzania.
WanaCCM hao walieleza kuwa usiku wa kuamkia Machi 10 mwaka huu watu wasiojulikana waliliunguza kwa makusudi Tawi lao hilo moto na kuweka matairi sehemu ya mlangoni na kuliunga paa pamoja na vifaa vyote vilivyomo ndani jambo waliloliita kuwa ni hujuma kwa ushahidi wa kimazingira.