Thursday , 7th May , 2015

Nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki zimetakiwa kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wadau wa maendeleo ikiwemo jumuiya ya ulaya kwa kudumisha amani na utulivu ili malengo ya kuwawezesha wananchi wake kuondokana na umaskini yaweze kufikiwa.

Balozi wa Jumuiya ya nchini Mh Filliberto Cerian Sebregondi

Akizungumza katika maadhimisho ya ushirikiano wa jumuiya ya ulaya na jumuiya ya Afrika Mashariki balozi wa jumuiya hiyo nchini Filliberto Cerian Sebregondi pamoja na kuelezea adhma ya jumuiya ya ulaya ya kuendelea kusaidia jumuiya ya Afrika Mashariki amesema yanayotokea nchini Burundi yanakatisha tamaa.

Aidha balozi Filliberto amesema pamoja na changamoto hizo jumuiya hiyo inatarajia kusaini mkataba wa msaada wa zaidi ya Eur bilion moja kwa ajili ya kusaidia huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi wa nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kwa upande wake naibu katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia mipango na miundombinu Dkt, Enorck Bukuku amesema misaada inayotolewa na jumuiya ya ulaya imeonekana wazi kupunguza matatizo ya wananchi wa nchi zote wanachama hasa kwenye sekta ya miundombinu .

Baadhi ya washiriki ambao ni vijana wa vyuo vikuu kutoka nchi wanachama wamesema jitihada za kuimarisha jumuiya bado zinahitajika kwani kinadharia yapo mabadiliko lakini hali halisi inaonesha kuwa changamoto bado ni kubwa.