Thursday , 2nd Jun , 2016

Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya EU EOM wamesema katika uchaguzi mkuu wa Tanzania uliofanyika mwaka jana kulikuwa na mapungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na Tume ya Uchaguzi nchini NEC kutokuwa na uwazi juu ya michakato ya kufanya maamuzi.

Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umoja wa Ulaya EU EOM umesema katika uchaguzi mkuu wa Tanzania uliofanyika mwaka Jana kulikuwa na mapungufu kadhaa ikiwa ni pamoja na Tume za Uchaguzi nchini NEC kutokuwa na uwazi juu ya michakato ya kufanya maamuzi.

Hayo yameelezwa na waangalizi hao, leo jijini Dar es Salaam wakati wakiwasilisha ripoti kamili ya Uchaguzi, pamoja na mapendekezo yao ya chaguzi zijazo.

Akizungumzia baadhi ya Changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, zilizoanishwa katika Ripoti hiyo, Muangalizi Mkuu wa Ujumbe wa Waangalizi wa Uchaguzi wa Umojà wa Ulaya EU ambaye pia ni mbunge wa Bunge la Ulaya, Judith Sergentini amesema maofisa wa kusimamia na kuendesha uchaguzi hawakupewa elimu ya kutosha na haikuwa kwa wakati.

Ripoti hiyo inaainisha kuwa uchaguzi wa mwaka jana ulikuwa na mwamko mkubwa kwa wapiga kura, ushindani kwa vyama vya siasa pamoja na wagombea hali ambayo ilihitaji maandalizi ya kutosha ili kuepuka dosari zilizojitokeza katika vituo vya kupigia kura.

Bi. Sergentini anasema ripoti hiyo inapendekeza serikali kuweka mipango itakayotoa fursa ya mgombea binafsi katika chaguzi zijazo, kuruhusu kupinga matokeo ya Rais Mahakamani, Haki ya vyama vya siasa kuunda umoja wa kiuchaguzi, kuendelezwa kwa muundo wa Kudumu Tume ya uchaguzi pamoja na kuandaliwa upya kwa mchakato wa uteuzi wa makamishna wa uchaguzi wa Tume za uchaguzi.

Akizungumzia Suala la Zanzibar, Bi.Sergentini anasema mchakato wa waandikishaji wapiga kura uangaliwe upya ili kuhakikisha ushirikishi zaidi pamoja kurejesha imani kwa wapiga kura kutokana na kurejewa kwa uchaguzi uliodaiwa kuchangiwa na dosari zilizojitokeza katika uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka Jana.