Tuesday , 7th Jul , 2015

Mamlaka ya Ukanda Maalum ya Uwekezaji EPZA, imeibuka mshindi wa kwanza katika tuzo za mhamasishaji bora wa biashara na uwekezaji kwenye maonesho ya 39 ya biashara ya kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Uwekezaji na Uhamasishaji wa EPZA, Zawadi Nanyaro

Akizungumza katika Maonesho hayo mkurugenzi wa uwekezaji na uhamasishaji wa EPZA, Zawadia Nanyaro amesema kupata tuzo hiyo ni matokeo ya kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha miundombinu imara ya kiuwekezaji nchini.

Ameongeza kuwa kazi kubwa ya Mamlaka hiyo ni kuandaa Mazingira mazuri na kuvutia wawekezaji ikiwemo kujenga miundo mbinu mizuri na kusaidia wawekezaji hatua za kufuata ili kupata maeneo mazuri ya kuwekeza.

Aidha Nanyaro amesema kuwa mradi mkubwa wa kiuwekezaji wa ekari 9000 unaotarajiwa kufanywa Bagamoyo Mkoani Pwani utazinduliwa Agosti mwaka huu na hivyo kubadilisha taswira ya mji mkongwe wa Bagamoyo.