Thursday , 11th Dec , 2014

Waziri wa Kazi na Ajira Gaudencia Kabaka amesema kuwa elimu ya Ufundi ikitiliwa mkazo inaweza kupunguza tatizo la ajira nchini kwa kuwawezesha vijana kuajiriwa na kujiajiri kupitia ujuzi walionao.

Waziri wa Kazi na Ajira Gaudencia Kabaka.

Akizungumza katika Kongamano lililoandaliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) na kufanyika jijini Arusha,Gaudencia ameeleza kuwa kada ya ufundi ina fursa za ajira kwa kuwa inashabihiana na mahitaji ya soko la ajira.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya VETA,Idrissa Mshoro amesema kuwa kongamano hilo linawakutanisha wadau mbali mbali wakiwemo wamiliki wa viwanda na waajiri kuona jinsi ambavyo wanaweza kuanisha maeneo ya kuzingatiwa kwenye mitaala ili elimu hiyo iendane na mahitaji halisi ya soko na kupanua wigo wa ajira.

Mkurugenzi Mkuu wa VETA ,Injinia Zebadiah Moshi amesema lengo la Kongamano hilo ni kupata mrejesho kwa waajiri ,wamiliki wa viwanda na wadau mbali mbali ili kuboresha elimu ya ufundi izidi kukidhi mahitaji ya soko.

Ukosefu wa Ajira ni tatizo sugu nchini na duniani kwa ujumla,Huenda tatizo hili likapunguzwa na Ongezeko la elimu ya ufundi ambayo itawasaidia vijana kuajiriwa na kujiajiri katika sekta rasmi na zisizo rasmi.