Friday , 5th Aug , 2016

Katika hali isiyo ya kawaida shirika la maji safi na maji taka DAWASCO jijini Dar Es Saaal na Pwani DAWASCO, limeingia mitini katika Ziara ya Naibu Waziri wa Mazingira na Muungano Mhe. Luhaga Mpina.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh.Luhaga Mpina akisikiliza kero za harufu kali za mabwawa ya maji taka kutoka kwa wana nchi yaliyopo Buguruni kwa Mnyamani jijini Dar es salaam mara baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa mazingira.

Ziara ya Naibu Waziri Mpina ililenga kutembelea miondombinu ya maji taka na maji safi Jijini Dar es Salaam na Pwani Leo.

Licha ya shirika hilo kupewa Taarifa ya Ziara ya Naibu waziri Mpina mwezi mmoja kabla limekaidi kwa kutoitikia wito huo hata kwa kumuwasilisha mtumishi mmoja kuwakilisha shirika hilo.

Akiongea kwa ukali baada ya kutembelea bomba la kusafirisha maji taka kwenda baharini la Ocean Road, Naibu Waziri Mpina amesema ubovu wa bomba hilo unatokana na kutokukarabatiwa kwa muda mrefu, unaonesha dhahiri kuwa DAWASCO wana Jeuri kwa Ikulu, kwa kutokulifanyia ukarabati kwa muda mrefu bomba hilo lililoko karibu na maeneo hayo.

Alipotembelea mabwawa ya maji taka ya Mabibo na Buguruni, Mhe Mpina Amesema pamoja na kuwa miondombinu hiyo inaelemewa na wingi wa wakazi wa Dar es Salaam, mamlaka husika zina wajibu wa kuyafanyia usafi mabwawa hayo lakini, hazijaonekana jitihada zozote za kufanya hivyo, na miondombinu hiyo inaonekana kutofanyiwa ukarabati kwa muda wa miezi sita.

Naibu Waziri Mpina amesisitiza kuwa ubovu na uchafu wa miundombinu hiyo unapelekea uchafuzi wa mazingira na hivyo kuhatarisha maisha ya wakazi wa maeneo hayo pamoja na viumbe hai wengine.

Akiongea kwa uchungu, mkazi mmoja wa Mabibo aliyekataa kutaja jina lake amesema
“Mabwawa haya ni ya Dawasco na hata tukitaka kuunganisha maji taka kwenye mabomba yao kuelekea kwenye mabwawa wana taka tuwalipe na tunafanya hivyo, wenye viwanda halikadhalika wanawalipa Dawasco kwa kupitisha maji taka yao katika miundombinu ya dawasco, lakini najiuliza, kwa nini wanakuwa wagumu kuyafanyia ukarabati au hata kusafisha tuu?" Amesema mkazi huyo

Ziara ya Naibu Waziri Mpina ya kukagua miundombinu ya DAWASCO leo Jijini Dar es Saalam ilihushisha maafisa kutoka DAWASA na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira NEMC na kuwaagiza NEMC, wapitie miradi yote inayosimamiwa na DAWASCO na kuona kama wanatenda haki katika kutoa huduma kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh.Luhaga Mpina akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kufanya ziara kukagua miundo mbinu ya Dawasco inayolalamikiwa na wana nchi kwa kutiririsha maji machafu sehemu za makazi, jijini Dar es salaam mapema hii leo.