Wednesday , 1st Oct , 2014

Serikali ya Tanzania inakamilisha uwekaji wa kamera maalumu za kubaini matukio yote ya uhalifu, ambapo mpaka kufikia Juni mwakani, vyombo vya ulinzi na usalama vitakuwa vinaweza kubaini matukio yote yanayofanyika katika mitaa jijini Dar es Salaam.

Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Rais wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua kipande cha barabara ya Mwenge Tegeta, chenye urefu wa kilomita 12.9, kilichojengwa kwa ushirikiano kati ya serikali ya Tanzania na Japan na kugharimu fedha za Tanzania shilingi bilioni 99.6.

Kwa mujibu wa rais Kikwete, ufungaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara na miundombinu ya usafirishaji, ambapo ameonya kuwa siku za wahalifu wanaopora, kuiba na kudhuru watu katika mitaa na barabara za jiji la Dar es Salaam sasa zinahesabika.

Aidha, rais Kikwete amewataka Watanzania kuachana na dhana potofu kuwa serikali inaweza kumaliza tatizo la msongamano wa magari katika mitaa ya katikati ya jiji la Dar es Salaam, na kwamba inachoweza kufanya hivi sasa ni kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.

Rais amefafanua kuwa tatizo tatizo la msongamano wa magari ni la kawaida kwa maeneo yenye shughuli nyingi katika miji mikuu mbali mbali duniani, na kwamba katika jiji la Dar es Salaam, serikali inakaribia kuanza kutumia usafiri wa majini kama sehemu ya kupunguza ukubwa wa tatizo hilo.