Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na Balozi wa Cuba nchini, Mhe. Jorge Luis Lopez Tormo,ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Akizungumza na Balozi Tormo, ofisini kwake, Magogoni jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu amemshukuru Balozi huyo, kwa Serikali ya Cuba kuendelea kusaidia Tanzania katika mapambano dhidi malaria kwa kusaidia ujenzi wa kiwanda cha kwanza Afrika cha viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria kilichopo, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani kinachosimamamiwa na Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC).
“Nawashukuru sana kwa namna mnavyosaidia kupambana na malaria, kupitia mradi huo mkubwa Afrika ambao unalenga kumaliza ugonjwa wa malaria,unaosababisha idadi kubwa ya vifo katika nchi yetu.” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Pia, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha raia wa Cuba kuja kuwekeza nchini hasa katika teknolojia. Na ameahidi kuendeleza uhusiano mwema ulipo baina ya nchi hizi mbili.
Waziri Mkuu ameendelea kwa kusema kuwa Cuba ni nchi iliyoendelea katika biashara, viwanda na uwekezaji na imefanikiwa kutoa bure huduma za kijamii ikiwemo afya, hivyo serikali ya Tanzania haina budi kujifunza kutoka kwao ili kutimiza azma yake ya kutoa bure huduma mbalimbali za kijamii kama ambavyo sasa inatolewa elimu bure.
Kwa upande wake, Balozi Tormo amesema kuwa pamoja na Serikali ya Cuba kusaidia kutoa wataalamu katika kujenga kiwanda hicho cha viuadudu vya kuua viluwiluwi wa mbu wanaoeneza ugonjwa wa malaria ambao utanufaisha pia nchi za jirani siku za usoni, wanapenda kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika kuzalisha wataalamu kupitia programu mbalimbali ikiwemo afya na elimu. Mfano progamu inayoendelea ya kubadilishana wataalamu katika kitivo cha madawa cha Chuo Kikuu Cha Zanzibari (SUZA).
“Tunaweza kuendeleza program za kujifunza lugha ya Kiswahili, kama hapo awali, hii ni njia nzuri na muhimu ya kuendeleza uhusiano wetu na watu kuelewa lugha zetu”, alisema Balozi Tormo.