Wednesday , 22nd Jun , 2016

Chuo Kikuu cha Tumaini tawi la Makumira kilichopo wilayani Arumeru, kimetoa Shilingi milioni kumi, kwa ajili ya ununuzi wa madawati miambili, kwa shule za Halmashauri ya Meru wilayani Arumeru.

Akizungumza jana wakati wa kukabidhi msaada huo kwa mkuu wa wilaya ya Arumeru Wilson Nkambaku mkuu wa chuo hicho Prof.Joseph Parsalau amesema wametoa msaada huo baada ya mkuu huyo wa wilaya kufika ofisini kwake na kuomba msaada kwa ajili ya madawati katika Halmshauri hiyo.

Amesema chuo hicho siyo kwamba ni tajiri lakini kimeona elimu ni jambo la msingi kwa watoto walioko mashuleni, hivyo ni vyema wakapatiwa mahitaji ya lazima kama madawati ili waweze kusoma katika mazingira mazuri badala ya kukaa chini.

Akimshukuru mkuu huyo wa chuo mara baada ya kupokea fedha hizo mbele ya watumishi, Mbunge na madiwani wa Halmashauri ya Meru Nkambaku amesema alilazimika kuomba madawati wiki iliyopita kutokana na Halmashauri hiyo kukabiliwa na ukosefu wa madawati.

Nkambaku amesema fedha hizo zitawezesha utengenezwaji wa madawati mia mbili na yatapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya madawati yanayohitajika.

Aidha ametumia fursa hiyo kumpongeza mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari pamoja na madiwani ambapo amekuwa mstari wa mbele katika harakati za kuhakikisha madawati yanapatikana kwa wakati kama rais alivyoagiza.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Meru Bakari Sajini amesema baada ya agizo la Rais walifanya ukaguzi wa madawati katika shule zote za Halmashauri hiyo na kubaini kuwa wana upungufu wa madawati 4,683 na kwamba mpaka sasa wamekamilisha madawati 4,303 na kwamba wamebakiza madawati 380 pekee.

Sajini amewataja baadhi wadau wengine ambao wamechangia madawati hayo kwa nyakati tofauti kuwa ni pamoja na hifadhi ya taifa ya Arusha(ANAPA) ambayo imechangia kiasi cha shilingi milioni 18, Chama Cha Mapinduzi (CCM) madawati 10, wakuu wa idara wa Halmshauri ambao kila mmoja amechangia dawati moja na mkuu wa wilaya Nkambaku ambaye amechangia madawati 10 .