Monday , 24th Aug , 2015

Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA mkoa wa Njombe kimemuwekea pingamizi mgombea wa Chama cha Mapindusi CCM, kiti cha ubunge jimbo la Njombe Kusini Edward Mwalongo, na kusema kuwa hawana imani na msimamizi wa uchaguzi msaidizi wa jimbo hilo.

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Njombe Ally Mhagama.

Akizungumza na kituo hiki mkoani Njombe mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Njombe Ally Mhagama amesema kuwa Chadema wamemuwekea pingamizi mgombea wa CCM ambaye katika fomu yake inadaiwa kuwa alijaza kuwa aliwahi kuhukumiwa kwa makosa ya jinai kitu kinacho mnyima sifa ya kuwa mgombea.

Mgombea wa Chadema kiti cha ubunge, Emmanuel Masonga amesema kuwa licha ya kuona kuwa mgombea wa CCM alijaza kuwa aliwahi kuhukumiwa lakini msimamizi wa uchaguzi msaidizi wa jimbo hilo ambaye ni mkurugenzi wa halmashauri ya mji mji Njombe alimrekebishia fomu hiyo siku ya Jumamosi majira ya saa 7 Alasiri na kuwa kitu ambacho ni kinyume na taratibu ambazo fomu ilitakiwa kujazwa na kukabidhiwa kwa tume siku ya Ijumaa saa kumi.

Amesema kuwa siku ya Jumapili wamepeleka mapingamizi tume ya uchaguzi makao makuu na kuwa katika ngazi ya jimbo wamepeleka nakala.

Kwa upande wake msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Njombe kusini Venance Msungu amesema kuwa siku ya Jumamosi walipokea pingamizi kutoka Chadema dhidi ya mgombea wa CCM ambapo waliwasilisha pingamizi alirekebisha makosa katika fomu hiyo.

Amesema kuwa kosa la mgombea huyo lilikuwa ni la kimakosa ya kawaida na kuwa kama wana uhakika na walicho kijaza basi walete uthibitisho wa kimahakama ambao unaeleza kuwa aliwahi kishitakiwa na kuwa watayapokea na kufanyia kazi.

Upande wa katibu wa CCM wilaya ya Njombe, Saadi Kimati, amesema kuwa katika ujazaji wa fomu kipengele hicho kilijazwa kimakosa na kuwa ndio maana sehemu ya kutoa maelekezo palibaki bila kutoa maelezo.

Alipo ulizwa ngombea wa CCM Edward Mwalongo ambaye amewekewa pingamizi na Chadema alisema kuwa hajapokea taarifa zozote kuhusiana na kuwapo kwa pingamizi hilo na anatarajia kama lipo kupokea kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi.

Kwa upande wa tume ya uchaguzi (NEC) kupitia Mwenyekiti wake Jaji Damian Lubuva amesema kuwa kwa malalamiko ya majimbo yatafika kwao kama hayatashugulikiwa kutoka katika jimbo husika.