Thursday , 25th Dec , 2014

Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) imetangaza matokeo ya jumla ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Desemba 14 na 21 mwaka huu huku Chama Cha Mapinduzi kikiwa hakijafanya vizuri katika matokeo hayo.

Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Khalist Luanda.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa wakati wa kutangaza matokeo hayo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kharist Luanda, alisema kwa mwaka huu ushiriki wa vyama vya siasa umekuwa mkubwa kutokana na vyama 15 kushiriki.

Amesema katika vyama 15 vilishiriki jumla ya vyama 11 vimepata wawakilishi na vingine 4 vikikosa kiti hata kimoja.

Aidha, Luanda alisema kuwa mwaka huu kulikuwapo na hamasa kwa wananchi katika uchaguzi huo ikilinganishwa na miaka iliyopita ambayo ulikuwa ukifanyika kienyeji na bila mvuto.

Luanda alisema licha ya vyama vya upinzani kupata viti vingi vya mitaa, vitongozi na vijiji ambavyo miaka iliyopita vilikuwa vinashikiliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama hicho tawala, kimeongoza.

Alisema katika nafasi ya wenyeviti wa vijiji,  CCM kimepata  9,378 (asilimia 79.81) wakati kwa vitongoji 48,447  (asilimia 79.83) na kwa mitaa  2,583 (asilimia 66.66.).

Kwa upande wa wajumbe serikali za vijiji na mitaa, CCM kimepata 100,436 (asilimia 80.24) na wajumbe wa viti maalum 66,147 (asilimia 82.13).

Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi vimefuatia kwa kuzoa viti vingi ambavyo vilikuwa vinashikiliwa na CCM hadi baada ya uchaguzi wa mwaka 2009.

Chadema kimeshika nafasi ya pili kwa kupata wenyeviti wa vijiji 1,754 (asilimia 14.93), vitongoji 9,145 (asilimia 15.07) huku kikipata mitaa 980   (asilimia 25.29).

Katika nafasi za wajumbe serikali za vijiji na mitaa kimepata 18,527 (asilimia 14.80) na wajumbe viti maalum  10,471 (asilimia 13).

Kilichofuatia ni CUF ambacho kwa nafasi ya wenyeviti wa vijiji kimepata viti 516 (asilimia 4.39), wenyeviti wa vitongoji 2,561 (asilimia 4.22) na  wenyeviti wa mitaa 266 (asilimia 6.86).

Katika nafasi ya wajumbe serikali za vijiji na mitaa  kimepata 5,395 (asilimia 4.31) na viti maalum  kimepata wajumbe 2,676 (asilimia 3.32).

NCCR-Mageuzi katika nafasi ya wenyeviti wa vijiji kimepata 67 (asilimia 0.57), wenyeviti wa vitongoji 339 (asilimia 0.56) na wenyeviti wa mitaa 28  (asilimia 0.72).Chama hicho kwa wajumbe serikali za vijiji na mitaa kimepata 598 (asilimia 0.48) na viti maalum 455 (asilimia 0.56).

Aidha, Luanda alivitaja vyama vingine kuwa ni TLP ambacho kwa wenyeviti wa vijiji kimepata viti 10 (asilimia 0.09), NLD wawili (asilimia 0.02), ACT wanane  (asilimia 0.07), UDP 14 (asilimia 0.12), NRA mmoja (asilimia 0.01) na kwamba vyama vilivyobaki havikupata uwakilishi.

Kwa upande wa wenyeviti wa vitongoji  TLP kimepata 55 (asilimia 0.09), NLD wawili (asilimia 0.00), ACT 72 (asilimia 0.12), UDP 54  (asilimia 0.09), APPT Maendeleo watatu (asilimia 0.00), NRA watatu (asilimia 0.00) na vyama vingine havikupata uwakilishi.

Luanda alisema kwa wenyeviti wa mitaa TLP kimepata mmoja (asilimia 0.03), ACT 12 (asilimia 0.31), UDP watatu (asilimia 0.08), NRA mmoja na UMD mmoja (asilimia 0.03).

Katika nafasi ya wajumbe serikali za vijiji TLP kimepata 62 (asilimia 0.05), NLD watatu (asilimia 0.00), ACT 106 (asilimia 0.08), APPT Maendeleo mmoja, Chaumma mmoja na NRA wanne (asilimia 0.00).

Mkurugenzi huyo alisema kwa upande wa wajumbe wa viti maalum, TLP 63 (asilimia 0.08), NLD mmoja (asilimia 0.00), ACT 57 (asilimia 0.07), UDP 43  (asilimia 0.05), APPT Maendeleo mmoja na Chaumma mmoja (asilimia 0.0).

Hata hivyo, Luanda  alisema matokeo hayo ni sawa na asilimia 99 ya maeneo yaliyofanya uchaguzi na kwamba bado kuna maeneo ambayo hayajafanya uchaguzi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo mapingamizi, karatasi kuchomwa moto, vifo na kuongeza kuwa hayawezi kubadilisha asilimia za kichama zilizopatikana kwa sasa.

Mkurugenzi huyo alisema kwa upande wa wajumbe wa viti maalum, TLP 63 (asilimia 0.08), NLD mmoja (asilimia 0.00), ACT 57 (asilimia 0.07), UDP 43 (asilimia 0.05), APPT Maendeleo mmoja na Chaumma mmoja (asilimia 0.0).

Hata hivyo, Luanda alisema matokeo hayo ni sawa na asilimia 99 ya maeneo yaliyofanya uchaguzi na kwamba bado kuna maeneo ambayo hayajafanya uchaguzi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwamo mapingamizi, karatasi kuchomwa moto, vifo na kuongeza kuwa hayawezi kubadilisha asilimia za kichama zilizopatikana kwa sasa.

Wiki iliyopita, CCM kupitia kwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, baada ya kutangazwa matokeo ya kwanza kabla yaw a marudio, alikiri kwamba ushindi wa chama hicho umepungua kwa asilimia 12 kutoka asilimia 96 za mwaka2009 hadi asilimia 84 zamwaka huu.

Nnauye alisema kuwa ingawa wapinzani wameshinda kwa asilimia 16, lakini ushindi huo siyo kigezo cha kufanya vizuri katika uchaguzi mkuu wa mwakani.