Wednesday , 2nd Jul , 2014

Naibu Waziri wa Fedha na uchumi Mwigulu Nchemba amefafanua kuhusu sakata la fedha katika akaunti ya Escrow ambapo amewataka Watanzania wasubiri ripoti ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG, ripoti ambayo amesema itaeleza ukweli.

Naibu waziri wa fedha na uchumi Mwigulu Nchemba.

Akizungumza kwenye mahojiano ya moja kwa moja na kipindi cha East Africa Breakfast Show cha East Africa Radio, mhe. Mwigulu amesema maneno mengi yamezungumzwa kuhusu namna malipo ya zaidi ya shilingi bilioni mia mbili yalivyolipwa kutoka katika akaunti hiyo na kwamba cha msingi ilikuwa ni kama fedha hizo zimelipiwa kodi, ambayo amesema ililipwa.

Kwa mujibu wa mhe. Mwigulu, kuibuka kwa sakata hilo na hata akaunti ya Escrow yenyewe ni utata ulioibuka baina ya wanahisa wa kampuni ya IPTL na kwamba iwapo kusingekuwa na tofauti hiyo, fedha hizo zingeshalipwa muda mrefu na pasingekuwepo na sakata linaloendelea hivi sasa.

Aidha, mhe. Mwigulu amesema serikali imekuwa ikuchukua hatua mbali mbali katika kudhibiti matumizi makubwa serikalini ikiwemo kupunguza asilimia tano katika funu la matumizi mengineyo kwenye wizara na taasisi mbali mbali.

Hatua nyingine kwa mujibu wa naibu waziri Mwigulu ni kupunguza matumizi ya magari ya kifahari ambapo wizara yake imeamua kukata takribani asilimia hamsini ya maombi ya ununuzi wa magari ya kifahari.

Naibu waziri huyo amewatupia lawama watendaji waandamizi kwa kuandaa bajeti aliyoiita ni ya kitajiri kutokana na kutozingatia hali halisi ya maisha ya Watanzania ambao wengi wao wana hali mbaya ya kiuchumi kiasi cha kutoweza kumudu hata mlo mmoja kwa siku.