Zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa kutumia mfumo wa BVR katika vituo zaidi ya 400 vya jimbo la Sengerema mkoani Mwanza lililoanza Juni 9 mwaka huu limeendelea kwa kusuasua kutokana na kasi ndogo ya uandikishaji pamoja na uchache wa mashine za BVR, hali ambayo imesababisha baadhi ya vituo kushindwa kabisa kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu ya wazee, akinamama wajawazito na watu wenye ulemavu.
Eatv imefanya ufuatiliaji wa zoezi hilo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura vilivyopo katika shule ya sekondari Nyampukano, kituo cha wajasiriamali, ofisi ya chama cha walimu wilayani Sengerema, chuo cha uuguzi Sengerema, shule ya msingi Sengerema, pamoja na kituo cha migombani na kushuhudia foleni ndefu za wapigakura, uchache wa mashine za kuandikishia, kasi ndogo ya waandikishaji na tatizo la baadhi ya mashine kushindwa kutambua alama za vidole- changamoto ambazo zinaweza kusababisha zoezi hilo kutokamilika kwa asilimia 100.
Mratibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA ) kanda ya ziwa victoria Robert Bujiku ambaye tangu kuanza kwa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura katika mikoa ya Kagera na Mwanza amekuwa akitembelea vituo mbalimbali ili kujionea hali ya uandikishaji inavyoendelea, amezungumzia kile alichokibaini katika jimbo la Sengerema.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Sengerema Marietha Kasongo ambaye pia ni afisa mwandikishaji wa wilaya hiyo amesema kuwa mashine 125 za BVR zilizotolewa na tume ya taifa ya uchaguzi katika wilaya hiyo, ana uhakika zitatosheleza kuandikisha wapigakura zaidi ya laki moja na kuongeza kuwa hakuna mwananchi yeyote mwenye sifa ya kuandikishwa atakayeachwa bila kuandikishwa katika muda wa siku 28 za zoezi hilo mkoani Mwanza.