Maafisa wa serikali za vitongoji, vijiji na uhamiaji wa wilaya za mpakani na Kenya wametakiwa kushirikiana na maafisa waandikishaji wa daftari la wapiga kura ili kuwabaini baadhi ya wananchi wenye uraia wa nchi mbili wanaoishi upande wa Tanzania ambao uchaguzi mkuu uliyopita wa mwaka 2013 walipiga kura nchini kenya.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama ametoa changamoto hiyo katika uzinduzi wa zoezi la uandikishaji wa daftari la wapiga kura katika mkoa huo katika manispasa ya Moshi baada ya kupokea taarifa kutoka wilaya za Rombo na Moshi vijijini.
Bw Gama amesema taarifa katika wilaya hizo zinaonyesha kuwepo kwa watu wa aina hiyo hivyo ni vema maafisa hao wakachukua tahadhari ili wasijiandikishe na kuwataka wananchi wa mkoa huo wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika wilaya zote.
Hata hivyo baadhi ya wananchi waliojitokeza katika kata za Kilimanjaro, Karanga na Soweto katika manispaa ya Moshi wameeleza kutoridhishwa kwao na kasi ndogo ya uandikishaji na utaratibu unaotumika katika zoezi hilo.


