Afisa anayehusika na Sera, Utafiti pamoja na machapisho wa TLS Bw. Stephen Msechu amesema hayo leo jijini Dar es Salaam, wakati wa mahojiano maalumu na East Africa Radio iliyotaka kufahamu nafasi ya kisheria katika kunusuru mchakato unaoendelea wa katiba mpya.
Aidha Msechu amesema wao kama wanasheria, wamechukua hatua kadhaa katika kuepusha kuvurugika kwa mchakato huo na kwamba hivi karibuni wanakusudia kukutana na jopo la majaji wa mahakama kuu na mahakama ya rufaa, kwa lengo la kuangalia vipengele vinavyohusu utoaji wa haki katika Rasimu ya pili ya katiba ili watoe ushauri wao kwa bunge maalumu la katiba.
Wakati huohuo, taasisi na asasi zinazotoa msaada wa kisheria nchini Tanzania zimetakiwa kusogeza huduma za msaada wa kisheria katika magereza na mahabusu mbali mbali nchini, mahali ambako kuna uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria.
Naibu waziri wa katiba na sheria Bi. Angela Kairuki amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea ofisi za chama cha wanasheria Tanganyika TLS kama sehemu ya ziara ya kutembelea idara na taasisi zilizo chini ya wizara ya katiba na sheria.
Kwa mujibu wa naibu waziri Kairuki, idadi kubwa ya Watanzania wanaotumikia vifungo na wanaosubiri hukumu, hawafahamu sheria, hatua aliyosema inahitaji huduma za msaada wa kisheria kwa ajili ya kuhakikisha wanapata haki yao ya msingi ya kusikilizwa na kuhudumiwa kama inavyoeleza ndani ya katiba.
Naye makamu wa Rais wa TLS, mwanasheria Flaviana Charles amesema kwa kulitambua suala hilo wameanzisha kitengo maalumu kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa watoto na katika kanda za mikoa.