Thursday , 22nd May , 2014

Mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam na dereva wa gari yenye namba za usajili T 910 CGR aina ya Toyota Noah, Abbas Matenga, amemwagiwa kitu kinachodhaniwa kuwa ni tindikali na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi na kisha kumpora baadhi ya vifurushi.

Kamanda Camilius Wambura,mkuu wa polisi mkoa wa Kinondoni, mkoa ambao tukio la leo mchana limetokea.

Tukio hilo limetokea muda mfupi uliopita katika barabara ya Coca Cola jijini Dar es Salaam wakati mtu huyo akitokea eneo la Shoppers Plaza Mikocheni kuelekea Mlimani City ambako ndiko sehemu ya mzigo huo ulikuwa ukipelekwa.

Akisimulia tukio hilo huku akilalamika maumivu makali, mtu huyo anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 50, amesema alisikia pikipiki iliyokuwa na watu hao ikiligonga gari lake na kwamba aliposhuka kwa lengo la kuangalia uharibifu uliotokea ndipo watu hao walipommwagia kimiminika hicho na kuchukua baadhi ya vifurushi na kutoweka navyo.