Wizara ya Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania imesema itatumia zaidi ya Shilingi Bilioni 187.5 kujenga miundombinu ya kituo cha mkongo wa taifa katika maeneo ya Kijitonyama jijini Dar es Salaam.
Imesema kuwa hicho kitakuwa ndicho kituo kikubwa cha mkongo kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati katika juhudi za kurahisishwa upatikanaji wa Interneti.
Hayo yamesema leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania Prof. Makame Mbarawa Mnyaa katika mkutano uliowakutanisha wataalam mbalimbali wa mawasiliano kutoka nchi mbalimbali za Afrika, China na Korea.
Prof. Mbarawa ameongeza kuwa kituo hicho kitahifadhi data za serikali na sekta binafsi kwa usimamizi wa serikali na kuhakikisha kituo hicho kinakuwa mahiri katika tTeknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa nchi za Afrika, kwa kuweka na kusimamia sheria za mitandao duniani.

