Thursday , 21st Aug , 2014

Benki ya Maendeleo kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika ya PTA Bank imesema Tanzania ina fursa kubwa ya kunufaika kiuchumi iwapo itatumia vizuri mikopo inayotolewa na benki hiyo.

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa PTA Bank Bw. Admassu Tadesse.

Aidha, imeelezwa kuwa Tanzania ni mojawapo kati ya nchi tano zinazonufaika kwa kiasi kikubwa na mikopo inayotolewa na benki hiyo kwa nchi zilizo katika jumuiya za maendeleo za kikanda zikiwemo zile za COMESA, SADC na ile ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki EAC.

Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo Bw. Admassu Tadesse, amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa siku mbili wa bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo ambao pamoja na mambo mengine utajadili mipango endelevu ya benki hiyo.

Tadesse amesema Tanzania imeweza kutumia vizuri mikopo inayotolewa na benki hiyo kiasi cha kuifanya iwe moja kati ya mataifa yanayokuja juu kiuchumi barani Afrika na kwamba kinachotakiwa ni kwa sekta binafsi nchini kujipanga kwa ajili ya kuendelea kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotolewa na benki hiyo.

Bw. Tadesse amesema kwa sasa hali ya kifedha ya benki hiyo ni nzuri na kwamba kuna kila dalili za benki hiyo kuwa moja ya taasisi kubwa za kifedha duniani kutokana na kuendelea kukua kwa mtaji wake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi Mwigullu Nchemba ameishukuru benki hiyo kutokana na kufadhili miradi kadhaa ya uwekezaji hapa nchini ukiwemo mradi wa upanuzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa naibu waziri Nchemba, kinachofuata sasa ni kwa sekta binafsi nchini kuandaa mawazo mazuri ya biashara na ambayo yanaweza kukopesheka ili wafanyabiashara hao wayapeleke mawazo yao kwenye benki hiyo ili wapatiwe mikopo.

Ametoa angalizo kuwa mawazo hayo yalenge kukuza miradi na biashara husika na sio mawazo ya biashara yenye mtazamo wa kushindwa kwa kutegemea dhamana ya serikali kulipa madeni punde biashara husika zitakapofilisika.