Thursday , 12th Feb , 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete amewaapisha Dkt. Hamisi Mwinyimvua kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara Fedha na Balozi wa Tanzania nchini Kenya John Haule katika hafla iliyofanyika leo Ikulu jijini Dar es salaam.

Akizungumzia nafasi yake ya sasa, Naibu Katibu Mkuu Wizara Fedha Dkt. Hamisi Mwinyimvua amemshukuru Rais kwa kumteua ili akaongeze nguvu katika Wizara ya Fedha kwa kuwa yeye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi.
 
“Naenda kuwa sehemu ya viongozi wa wizara, hivyo naenda kuungana na timu ya viongozi waliopo ili niweze kuchangia kukuza uchumi wa nchi yetu” alisema Dkt. Mwinyimvua.
 
 Dkt. Mwinyimvua amesema kuwa atashirikiana na viongozi waliopo katika wizara ya Fedha ikizingatiwa wapo Waziri, Manaibu Waziri, Katibu Mkuu, Manaibu Katibu Wakuu na watumishi wa Wizara nzima.
 
Aidha, Balozi Haule amekuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.