Wednesday , 14th Jan , 2015

Balozi wa Algeria ambaye aliyemaliza muda wake wa utumishi katika Tanzania, Mheshimiwa Tabat Jallouh amewatakia Watanzania mwaka wa mafanikio, amani na utulivu wa 2015

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Balozi wa Algeria nchini Tanzania, Mhe. Tabat Jallouh , wakati alipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, leo Desemba 30, 2014 kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini

Balozi wa Algeria ambaye aliyemaliza muda wake wa utumishi katika Tanzania, Mheshimiwa Tabat Jallouh amewatakia Watanzania mwaka wa mafanikio, amani na utulivu wa 2015, kwa kadri nchi inavyopitia katika mabadiliko makubwa ya kisiasa kwa njia ya kura ya maoni ya Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu.

Mheshimiwa Jallouh alitoa salamu zake hizo kwa Watanzania usiku wa kuamkia leo, Jumatano, Januari 14, 2015, wakati alipokuwa anaagana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.

Balozi Jallouh alimwambia Rais Kikwete kuwa anasikitika kuondoka mapema bila kuwa shuhuda na shahidi wa matukio hayo muhimu katika historia na uhai wa taifa la Tanzania.

“Nakutakia wewe binafsi, Mheshimiwa Rais na kupitia kwako, Watanzania wote, mwaka wenye utulivu, mafanikio na amani kwa kadri nchi inavyopita kipindi cha kutunga Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu. Ni matukio muhimu sana katika historia na uhai wa taifa la Tanzania,” alisema Balozi Jallouh, ambaye pia alimtakia Rais Kikwete maisha marefu na shughuli zenye mafanikio baada ya kustaafu.

Balozi Jallouh ambaye Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza Kusini mwa Jangwa la Sahara kuitumikia katika utumishi wake wa kibalozi, amekuwa Balozi wa Algeria katika Tanzania kwa miaka mitano.

Naye Rais Kikwete amemshukuru Balozi Jallouh kwa kuinua kwa kiwango kikubwa uhusiano wa Tanzania na Algeria. “Tunakushukuru kwa utumishi wako, tunakushukuru kwa kutuunga mkono, tumekuwa marafiki wa miaka mingi lakini wewe umetoa mchango wa pekee. Tutakukumbuka daima.”