Saturday , 25th Jul , 2015

Timu ya Azam FC imetinga katika hatua robo fainali ya Kombe la Kagame kwa kishindo baada ya kuibuka na ushindi Mnono wa Magoli 5 kwa bila dhidi ya Timu ya Adama City FC kutoka nchini Ethiopia.

Kikosi cha wanalambalamba AZAM FC.

Hadi kipindi cha Kwanza kinamalizika Azam FC ilikuwa ikiongoza kwa magoli 3 kwa bila mawili yakiwa yamefungwa na Kipre Cheche na lile la Farid Musa na kipindi cha pili kuongeza mabao mengine mawili kupitia kwa Mudathri Yahaya na Agrey Moriss.

Hata hivyo Adama FC walimaliza mchezo huo wakiwa na Upungufu wa wachezaji wawili baada ya Eshutu Mema kupewa kadi nyekundu ya moja kwa moja na Moges Tedese akipewa kadi ya pili ya Njano.

Nayo Timu ya KCCA ya kutoka Uganda imeweza kusonga mbele katika kundi hilo baada ya kuilaza timu ya Malakia kwa goli moja kwa bila goli lililofungwa na Ivan Sserukuma.

Michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati kombe la Kagame inatarajiwa kumalizika kesho katika hatua ya makundi kwa kuwakutanisha mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Soka Tanzania Yanga dhidi ya Khartoum ukitanguliwa na mchezo kati ya Gor Mahia na Telecom.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu mkuu wa Shirikisho la Soka nchini TFF, Mwesigwa Celestine amesema, timu zilizotolewa katika michuano hiyo zimeshaanza kuondoka ambapo baadhi ya timu zilipata changamoto mbalimbali kuhusu usafiri ambapo zilitatuliwa.