Monday , 9th Nov , 2015

Chama cha waajiri nchini Tanzania (ATE), kimeorodhesha baadhi ya mambo yanayotakiwa kufanyiwa kazi na serikali ya Rais Dkt. John Magufuli ili kuleta tija kazini na kuboresha mazingira ya kazi miongoni mwa wafanyakazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waajiri nchini (ATE) Dkt Aggrey Mlimuka.

Akizungumza jijini Mwanza mwishoni mwa wiki baada ya kufungua ofisi ya kanda, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Dkt. Aggrey Mlimuka amesema serikali ya Magufuli inapaswa kujielekeza zaidi katika kushughulikia suala la mazingira ya kibiashara ndani ya taasisi ya Sekta binafsi ili kuvutia uwekezaji nchini.

Aidha Dkt. Mlimuka ameongeza kuwa mategemeo ya waajiri wengi yapo kwa Rais Magufuli ambaye aliahidi wakati wa kampeni kuwa sekta binafsi itaangaliwa sambamba na waajiri wao.

Amesema mikataba ya ajira inatakiwa kuangaliwa ili kuendana na soko la ajira pamoja na kuangalia saa za kufanya kazi kwa mwezi na taratibu za kuachishwa waajiriwa kwenye ajira.