Friday , 10th Jul , 2015

Mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha DC, Wilayani Arumeru, Fidelis Lumato, amesema zoezi la uandikishwaji wapiga kura kwa kutumia mashine za Biometric Voters Registration BVR, linaendelea vizuri katika halmashauri yake na hadi sasa wamevuka lengo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha DC, Wilayani Arumeru, Fidelis Lumato,

Akizungumza jana katika kikao cha baraza la mwisho la halmashauri, muda mfupi kabla ya kuvunjwa kwa baraza hilo, Lumato amesema zoezi hilo lilianza Juni 20 mwaka huu katika halmashauri yake na litaenda katika awamu nne, ambapo awamu ya tatu itakwenda kata sita na nne itamaliziwa kata saba.

Lumato amesema kuwa mpaka sasa wameandikisha wapiga kura 76,000 na kuvuka lengo la kuandikisha wapiga kura 73,000 katika awamu mbili kwenye kata 14.

Lumato amesema endapo zoezi litaenda kama linavyoendeshwa kwa sasa kwa kuandikisha wapiga kura 150 hadi 200 kwa siku, wanatarajia kuwafikia wapiga kura zaidi ya 300,000.

Aidha ameomba wananchi wanaposikia daftari limefika katika maeneo yao wasiende wote siku ya kwanza, wapishane maana linakaa kwa siku saba katika kata moja, hivyo hakuna sababu ya kusukumana siku moja.

Amesema vijana wanaoandikisha ni wazoefu wa mashine hizo na wanaandikisha watu wengi kadri inavyowezekana, hivyo hakuna sababu ya wananchi kupata hofu ya kutoandikishwa.

Pia amewaomba wananchi wa maeneo yaliohamishwa kama ya kijiji cha Olligirai kimetolewa kata ya Olturmet na kuhamishiwa kata ya Kiutu na kijiji cha Olkokola kilichokuwa kata ya olkokola kimehamishiwa kata ya Olmanyatta, wazingatie maagizo ya waandikishaji kwa kujiandikisha maeneo wanayostahili.

Hata hivyo ametumia nafasi hiyo kuagiza viongozi wa mitaa, vijiji, kata ili kuzuia watu wanaotoka maeneo ya Halmashauri ya Jiji la Arusha kuja kujiandikisha maeneo yao.