Wednesday , 31st Dec , 2014

Jeshi la polisi mkoani Morogoro limemtia mbaroni mtuhumiwa mwenye silaha aliyekuwa akitaka kwenda kufanya uhalifu.

Silaha zilizokamatwa

Jeshi la polisi mkoani Morogoro limeendelea na operesheni shirikishi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, askari wa hifadhi ya taifa TANAPA, hifadhi ya mikumi na wananchi ambapo wamemtia mbaroni mtuhumiwa mwenye silaha aliyekuwa akitaka kwenda kufanya uhalifu.

Katika tukio lililothibitishwa na kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Leonard Paul, mtuhumiwa huyo Juma Salum (33) mkazi wa kijiji cha Mbamba Kitangili wilayani Mvomero, amekamatwa katika eneo hilo na askari wa hifadhi ya TANAPA, akiwa na silaha mbili aina ya Mark IV yenye namba za usajili PF 308068 pamoja na Gobore akidaiwa kujiandaa kwenda kufanya uhalifu.

Mkuu wa idara ya ulinzi wa hifadhi  ya mikumi, ameahidi kuwa wataendelea kutoa ushirikiano ili kuzuia na  kukomesha matukio ya ujangili na tayari wameanzisha mkakati wa kuwafuatilia na kuwakamata majangili wote.

Katika hatua nyingine jeshi la polisi mkoani morogoro limewaonya na kuwatahadharisha wale wote wanao panga kufanya uhalifu siku ya mwaka mpya, kuacha kufanya hivyo, kwani wamejipanga kukabiliana nao na kuwachukulia hatua kali za kisheria na kutoa wito kwa  wazazi na walezi kuwalinda na kuwakataza watoto kwenda kwenye kumbi za starehe siku hiyo.